Katika nchi ambayo biashara ndogo na kati (SMEs) ndio uti wa mgongo wa uchumi, ni muhimu sana kutambua na kushughulikia changamoto zinazokabili biashara hizi.
Nilipata fursa ya kufanya kazi na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) katika Mradi wa Kusaidia Mnyororo wa Thamani wa Ufugaji Nyuki nchini Tanzania, (BEVAC). Uzoefu huu umenipa mwanga kuhusu uwezo wa Biashara ndogo na Kati katika kukuza uchumi. Lakini kubwa zaidi, ni uhitaji wa jitihada za haraka na za makusudi za kuwawezesha wafanyabiashara hawa kidigitali.
Mradi wa BEVAC
Mradi wa BEVAC, ni juhudi za ushirikiano kati ya ITC, TANTRADE, Umoja wa Ulaya, na Enabel. Unalenga katika kuleta mabadiliko katika sekta ya ufugaji nyuki nchini Tanzania. Mpango huo unalenga kuongeza ubora wa bidhaa za ufugaji nyuki, kuongeza uzalishaji katika sekta hii, na kuinua thamani ya bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.
Safari yangu katika Mradi wa BEVAC ilihusisha kufanya kazi kwa karibu na Biashara Ndogo na Kati (SMEs) 19 za ufugaji nyuki. Hawakuwa na shauku ya ufugaji nyuki tu, bali pia walikuwa na shauku ya kujifunza na kukua zaidi.
Tuliwapa mafunzo ya kina na usaidizi wa vitendo. Tuliangalia vipengele mbalimbali vya biashara zao, kuanzia kwenye Chapa (Brand) Masoko (Marketing) hadi Uzalishaji (Production) na Udhibiti wa Ubora (Quality Control).

Faida ya Kuwezesha Biashara Ndogo na Kati Nchini
Mradi wa BEVAC umekuwa zaidi ya programu ya mafunzo kwa Biashara Ndogo na Kati nchini. Kutokana na uzoefu wangu nilioupata, mradi huu ni ushahidi wa umuhimu wa kuwezesha biashara hizi kufanikiwa katika:.
- Ukuaji wa Uchumi: Biashara za Kati na Ndogo zina nafasi kubwa katika maendeleo ya kiuchumi. Nchini Tanzania, ambapo sehemu kubwa ya watu wanategemea kilimo na shughuli zinazohusiana na kilimo, kuwezesha bishara hizi kuna athari chanya kwa jamii. Kadiri zinapostawi, zinatengeneza ajira, kuchochea uchumi wa ndani, na hivyo kuchangia katika kupunguza umaskini.
- Ushindani wa Kimataifa: Kama zikipata usaidizi na mafunzo sahihi, Biashara Ndogo na Kati (SMEs) nchini Tanzania, zinaweza kushindana katika kiwango cha kimataifa. Mradi wa BEVAC unalenga kuzipa biashara hizi ujuzi na maarifa yanayohitajika ili kufikia viwango vya kimataifa, kufikia masoko ya kimataifa, na kuzifanya zijikite zaidi katika sekta ya ufugaji nyuki.
- Ubunifu na Ustahimilivu: Biashara hizi zinajulikana kwa ari yao ya ubunifu, wa bidhaa na masoko. Hivo, kwa kuwawezesha, tunahimiza maendeleo ya mawazo mapya, bidhaa na mbinu za kufikia masoko. Hii, kwa upande wake, inakuza ustahimilivu wao katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuzalishaji na kimasoko, kama vile mabadiliko ya hali ya hewa na mabadiliko ya kiuchumi.
- Maendeleo ya Jamii: Biashara Ndogo na Kati (SMEs) wamejikita sana katika jamii zao za karibu. Mara nyingi hutafuta bidhaa kama asali n.k, kutoka kwa wazalishaji wa ndani na kisha kuziwekesha katika maeneo yao mikoani. Mfano mzuri, wafanyabiashara wengi wa asali hununua asali kutoka mikoa kama Tabora na Singida na kisha kupeleka mikoani na kufungasha na kuuza huko. Hii inamanisha kuwa kuwezesha Biashara Ndogo na Kati (SMEs) kunamaanisha kuwezesha jamii, na hivyo kuunda na kukuza mzunguko mzuri wa maendeleo.

Kwa Nini Nguvu Kubwa Zaidi Inahitajika
Japokuwa uzoefu wangu na kufanya kazi katika mradi huu umekuwa wa kuvutia, lakini pia umenifumbua macho kuona kwamba nguvu zaidi inahitajika ili kuwezesha Biashara Ndogo na Kati (SMEs) nchini Tanzania. Hii ndio sababu:
- Rasilimali chache: Biashara nyingi zinakabiliwa na vikwazo vya mtaji mdogo, teknolojia na mafunzo. Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kimataifa lazima yaelekeze rasilimali zaidi katika programu kama BEVAC ili kuziba mapengo haya.
- Ufikiaji wa Soko: Biashara hizi pia zinapata changamoto kubwa kufikia masoko makubwa zaidi. Juhudi za dhati zinapaswa kufanywa ili kurahisisha kanuni za biashara, kupunguza vizuizi vya biashara, na kuongeza majukwaa zaidi kwa Biashara hizi kuonyesha bidhaa zao kwa masoko ya kimataifa.
- Kuwajengea Uwezo: Mafunzo endelevu na programu za kuwajengea uwezo wafanyabiashara hawa ni muhimu. Biashara hizi zinahitaji usaidizi wenye mwendelezo ili kukabiliana na mabadiliko ya mienendo ya soko, kushikilia teknolojia za kidijitali, na kuboresha ushindani wao kwa wapinzani wa ndani na nje ya nchi.
- Usaidizi wa Sera: Serikali inapaswa kuunda na kuboresha mazingira wezeshi kwa Biashara hizi kupitia sera na kanuni zinazofaa. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuna upatikanaji rahisi wa vibali, motisha ya kodi, na kukuza elimu ya ujasiriamali mara kwa mara.
Mradi wa BEVAC umeangazia uwezo mkubwa wa Wafanyabiashara Ndogo na Kati (SMEs) nchini Tanzania na uhitaji wa lazima wa kuwawezesha. Biashara hizi sio tu vitega uchumi; ni sehemu muhimu za ukuaji, uvumbuzi, na maendeleo ya jamii. Tunaposonga mbele, kiuchumi na kidigitali, tuongeze juhudi za kusaidia na kulea Biashara hizi; tukitambua kuwa mafanikio yao yanafungamana na ustawi wa taifa letu. Ni wakati wa kuwekeza nguvu zaidi katika kuwezesha Biashara Ndogo na wale wa Kati, kufungua uwezo wao kamili, na kukuza ukuaji wa uchumi nchini.
